Wednesday, 20 August 2014

MILLEN HAPPINESS MAGESE: ASIMULIA AMBAVYO HAWEZI KUBEBA UJAUZITO, ASEMA YUPO TAYARI KUASILI


Na Martha Mboma (ANAJIANDAA, anaonekana kuwa ni mtu mwenye hisia sana kabla ya kuanza kuzungumza, anamuuliza jambo Lucy Ngongoseke maarufu kwa jina la Lucy Kiwele ambaye anamwambia ajikaze azungumze, baada ya sekunde kadhaa anaanza kujielezea…)
Naitwa Millen Happiness Magese ni mrembo wa Tanzania na Miss Tanzania wa mwaka 2001, kwa sasa nafanya kazi za mitindo nchini Marekani, kabla sijafika huko nilifanya kazi hiyo Afrika Kusini kwa miaka takribani nane.
Nipo chini ya Kampuni ya Ford Models, nilisaini mkataba wa miaka minne na baada ya hapo nikasaini tena miaka miwili na ndiyo nilipo mpaka sasa.

Miss Tanzania Mwaka 2001, Happiness Millen Magese akiwa ndani ya Global.


Millen Magese Foundation
Hii ni taasisi ambayo lengo kubwa ni kutoa msisitizo katika elimu. Suala hili linanihusu binafsi na ndiyo maana nalifanya kwa moyo, hapa Tanzania nimeanza na Mtwara baada ya hapo nitaendelea mikoa mingine. Hata nilipokuwa Miss Tanzania nililifanyia kazi suala hili na nilikuwa na ndoto nyingi.
Nakumbuka nilikuta watoto wanakaa chini wakiwa darasani, miaka 12 baadaye nimerejea Mtwara nimekuta hali ileile, pia kuna masuala ya afya ambapo tumeanza na ugonjwa wa endometriosis.
Mimi na timu yangu tumetembea sehemu nyingi ikiwemo Basata kutafuta maana halisi ya Kiswahili ya jina hilo la endometriosis lakini bado hatujapata, ila naamini baada ya muda tutalipata.
Happiness Millen Magese akijifuta machozi wakati akielezea alivyoteseka kupata mtoto.
Hili ni suala la maumivu ya tumbo kwa wanawake, siwezi kulielezea kiundani kwa kuwa mimi siyo daktari, lakini nimeshazungumza na madaktari wa Muhimbili na wananisaidia kutoa elimu zaidi kuhusu huu ugonjwa huo.
Kukosa uwezo wa kubeba mimba
Inawezekana wapo wanaosikia juu-juu au hawafahamu kabisa juu ya ugonjwa huo na tatizo nililonalo. Nimeamua kuelezea suala hili na kutoa elimu hii kwa kuwa mimi ni mwathirika mkubwa wa matatizo hayo ya endometriosis, ndiyo maana sipendi kuona jamii yangu ikipotea na kuathirika kama nilivyoathirika.
Nimefanyia oparesheni mara 12 kiasi kwamba mpaka sasa mirija yangu ya uzazi imeziba, upande wangu mmoja wa ovary haufanyi kazi, kwa hiyo ile ndoto yangu ya kupata mtoto imeyeyuka, siwezi tena kubeba ujauzito katika hali ya kawaida kama wanawake wengine.
Ndiyo maana nimeamua kuja Tanzania kulielezea zaidi suala hili, naomba vyombo vya habari, serikali kujitokeza kunisaidia kuwaelimisha Watanzania juu ya endometriosis…
(Anashikwa na kwikwi, anainama, anatoa machozi, anaendelea kuzungumza lakini anashindwa kumaliza kila sentensi anayoitamka, anaendelea kutamka maneno haya kwa taabu sana, huku akijizuia kuendelea kulia…)
Suala hili ni la mwanamke lakini linawahusu watu wote, ninachoamini ukimsaidia mwanamke utakuwa umeisaidia dunia nzima, mwanamke ni nguzo katika nyumba, kwa kweli hili ni suala ambalo wababa, wakaka, viongozi wanatakiwa kulizungumzia kiundani.
(Anashindwa kuendelea kuzungumza, anainama anafuta machozi. Lucy ambaye yupo pembeni yake, anampa kitambaa, anajifuta machozi, Millen anaendelea kuwa kimya kwa dakika kadhaa.)
(Millen anaendelea) Ndoto ya mwanaume ni kuona mkewe anampatia mtoto, na mwanamke pia ana ndoto ya kumpa mumewe mtoto, hivyo kwangu hicho kitu hakipo tena.
Nawapa moyo wanawake wenzangu wote ambao hawawezi kupata mtoto kwa njia ya kawaida, lakini nawashauri kuwa kuna njia nyingine nyingi, mfano kubebewa mimba, kupandikiza mbegu au kuasili mtoto.
Nimeficha suala hili kwa miaka mingi, japo kuna watu wangu wa karibu wanalijua hilo kitambo, ningependa suala hili liongelewe kwa uwazi. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wanawake milioni 176 dunia nzima wanakumbwa na tatizo hili.
Najua mila na desturi zetu zinafanya ugumu wa suala hili kuzungumzwa hadharani, lakini inafikia hatua tubadilike. Unakuta binti anapoanza kukua anaambiwa maumivu ya tumbo kwa mwanamke ni jambo la kawaida na avumilie, lakini hajui kuwa huo ndiyo mwanzo wa kuingia kwenye tatizo la endometriosis.
Natoa changamoto kwa mabinti wadogo, ukiona maumivu yanazidi ni vema ukawaona wahusika, mimi nilianza kuumwa tangu nikiwa nina umri wa miaka 13, leo hii nina miaka 35 na ndiyo hivyo siwezi tena kupata mtoto.
Neno langu kwa wazazi ni kuwa mkiona watoto wenu wanalalamika maumivu ya tumbo, wapelekeni hospitali, hata kama wakipewa vidonge vya uzazi, msione aibu. Mimi sikupata nafasi hiyo lakini sipendi wengine wawe waathirika wakati inawezekana kutibika mapema.
Najua ili kugundulika unaumwa endometriosis kuna vipimo vyake maalum na ni gharama ndiyo maana nawaambia serikali na jamii yote kuwa hili ni tatizo la taifa, sifanyi hivi kwa kuwa nataka kuonekana au nijipatie umaarufu, hapana hili ni tatizo la kila mtu.
Naomba nitaje majina machache kwa ajili ya kusaidiana nami katika kuielimisha jamii, Diamond Platinumz, wewe una sauti inayosikika, unaweza ukatunga wimbo kwa ajili ya hii kitu na nitakubali kushiriki bure kwenye video yako.
Wema Sepetu, wewe una mguso kwa watu wengi, zungumza nao kuhusu suala hili, Jokate, Nancy Sumary, Lady Jaydee, Mwasiti, Lulu, Lina na wengine wengi mnaweza kutumia umaarufu wenu kuielimisha jamii.
Yawezekana labda sauti yangu haina nguvu kubwa kama ilivyo ninyi kwenye kizazi chenu cha sasa.
Binafsi kuna hatua nilikuwa nachomwa sindano 63 ndani ya siku 22, ambapo kila siku nilichomwa sindano tatu zote nikichomwa tumboni, maumivu yake ni makali, nimeteseka sana.
Nimejaribu kila njia lakini ikashindikana, nimejaribu tena na tena mpaka nikachoka, inavyoonekana hili suala liliniathiri kwa kiwango cha juu.
Namini nitaasili tu mtoto, na ninaomba Mungu anisaidie mwanangu huyo asipate matatizo kama niliyopata mimi, ikitokea nikapata mtoto wa kike.
Changamoto
Unajua kazi zetu hizi unatakiwa uendelee kuwepo kwenye fani muda wote, mimi nilikuwa nikifanyiwa oparesheni nalazimika kupumzika kwa miezi mitatu, sasa hapo kipindi hicho ukitoka tu wenzako wanaingia, hiyo ilinipa wakati mgumu sana lakini nashukuru nilipata waajiri ambao walinielewa.
Natoa wito kwa waajiri na wanafamilia, kukiwa na mwanamke ambaye anakuwa na maumivu ya tumbo, mfano matatizo kama ya kwangu, muwape nafasi wakihitaji kupumzika na msiwatupe maana wanaweza kujikuta wanafanya vitu kuwafurahisha ninyi kisha wao wanaumia ndani kwa ndani.
GPL

No comments: