Monday 28 September 2015

HAKI YA MAMA NYOSO SIO MZIMA, AMDHALILISHA BOCCO MCHANA KWEUPE


Kunradhi kwa picha hii; Juma Nyosso (kushoto) akimdhalilisha mchezaji mwenzake, John Bocco mbele ya refa aliyekuwa akisuluhisha mgogoro wa wachezaji wa timu hizo
 
BEKI na Nahodha wa Mbeya City, Juma Said Nyosso kwa mara nyingine leo amefanya kitendo cha udhalilishaji dhidi ya wachezaji wenzake, baada ya kumtomasa makalio, Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco.
Tukio hilo limetokea leo kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji Azam FC na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Nyosso alitumia mwanya wa refa Martin Saanya kutatua mgogoro baina ya wachezaji wa timu hizo, na kumtomasa mwenzake nyuma.
Na Bocco alionyesha utulivu na ustaarabu wa hali ya juu licha ya kuonyesha dalili zote za kukasirishwa na kitendo hicho, kwani alimfuata refa Martin Saanya kuwasilisha malalamiko yake.
Saanya hakuonekana kuyatilia mkazo malalamiko ya Bocco, ambaye alipandisha hasira na kutaka kumpiga Nyosso kama si refa huyo kuwatenganisha.
Benchi la Ufundi la Azam FC lilipeleka ushahidi wa picha kwa refa wa akiba, Soud Lila wa Dar es Salaam pia, ambaye alitoa maelekezo picha hizo zipelekwe kwa Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Iddi Mshangama.
Tukio hilo lilionekana kabisa kumnyima raha Bocco na kushindwa kucheza katika kiwango chake kuanzia hapo, ingawa Azam FC ilifanikiwa kushinda 2-1.
Hii inakuwa mara ya tatu kwa Nyosso kuonekana akifanya hivyo uwanjani, mara ya kwanza akiwa Ashanti United mwaka 2007 alimfanyia hivyo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Jospeh Kaniki aliyejibu kwa kumpiga ngumi hali iliyomponza kufungiwa na TFF.
Refa Martin Saanya akiwatenganisha Bocco na Nyosso (kulia) wasipigane

Nyosso na Bocco wakirushiana maneno mbele ya refa
Mwishowe Nyosso alionekana kama kumuomba msamaha Bocco

Akarudia tena msimu uliopita akiwa Mbeya City, alipomtomasa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Elias Maguri. Kutokana na ushahidi wa picha za magazeti, Nyosso alifungiwa mechi sita na TFF.
Huku wengi wakidhani kwamba adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake na hataweza kurudia tena, leo Nyosso ameonyesha yeye ni ‘nunda’, kwa kurudia tena baada ya kumdhalilkisha Bocco.
Wachezaji wote wa Azam FC wamekasirishwa na kitendo cha Nyosso na kiungo wa timu hiyo, Himid Mao amesema mchezaji mwenzao huyo si wa kumvumilia tena. 
Azam FC leo imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 2-1 Mbeya City.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Martin Saanya wa Morogoro, aliyesaidiwa na Julius Kasitu wa Shinyanga na Sylvester Mwanga wa Kilimanjaro, mabao ya Azam FC yalifungwa na 
kiungo Mudathir Yahya Abbas dakika ya 10 na mshambuliaji Kipre Herman Tchetche dakika ya 52, wakati la Mbeya City lilifungwa na Raphael Alpha dakika ya 56.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC ifikishe pointi 12, sawa na Mtibwa Sugar na Yanga SC, zikifuatiwa na Simba SC yenye pointi tisa.

No comments: